Rais Uhuru Kenyatta Aihimiza Ufaransa Kuunga Mkono Juhudi Za Kenya Za Kudumisha Amani

Rais Uhuru Kenyatta ameihimiza ufaransa kuunga mkono juhudi za Kenya za kudumisha amani na uthabiti katika kanda hii. Rais alisema kuwa Kenya inatazamia kushirikiana zaidi na washirika wake wa kimaendeleo katika kudumisha usalama hasa nchini Sudan kusini, Somalia na Burundi. Rais Kenyatta aliyasema haya leo wakati wa mkutano na waziri wa mashauri ya nchi za kigeni wa ufaransa Jean-Marc Ayrault aliyemtembelea ikuluni. Akimwarifu waziri huyo kuhusu hali ya usalama katika kanda hii rais alisema kuwa mkutano maalum wa shirika la IGAD utaandaliwa jijini Addis Ababa, Ethiopia mwishoni mwa juma hili kuamua msimamo wa kanda hii kuhusu Sudan kusini. Na kuhusu Somalia, rais Kenyatta alielezea wasiwasi wake kuhusiana na hatua ya muungano wa ulaya ya kukomesha usaidizi wake kwa ujumbe wa AMISOM. Ayrault alisema ufaransa inaunga mkono nchi hii na majirani zake katika juhudi za kuhakikisha amani kwenye kanda hii. Alipongeza jukumu la nchi hii katika kurejesha uthabiti na kuzijenga upya nchi za Somalia na Sudan kusini.