Rais Uhuru Kenyatta Ahudhuria Kongamano La Kiuchumi Rwanda

Rais Uhuru Kenyatta yuko mjini Kigali, Rwanda kuhudhuria kikao cha-26 cha kongamano la kiuchumi duniani. Kongamano hilo linaloangazia ushirikishi kwa raslimali za bara la Afrika kupitia mfumo wa dijitali linahudhuriwa na maelfu ya watu mashuhuri duniani wakiwemo wajasiriamali, wakuu wa mashirika ya kimataifa, waratibu sera na viongozi wa nchi kadhaa. Aidha kongamano hilo linatoa fulsa ya kuafikia mapatano baina ya sekta ya kibinafsi barani Afrika, ile ya umma na mashirika ya kijamii kwa lengo la kuchochea ustawi wa kiuchumi, kukabiliana na changamoto za kiuchumi barani humu, kuhamasisha kuhusu mahitaji ya wadau mbali mbali na kufanikisha ushirikiano kwenye nyanja muhimu. Rais Kenyatta anatarajiwa kufunga kikao cha kongamano hilo kuhusu fulsa za uwekezaji barani Afrika. Kikao hicho kilichotokana na wazo la Jumuia ya Afrika, Kongamano la kiuchumi duniani na shirika la NEPAD kinabainisha fulsa zilizopo za uwekezaji wa kibinafsi katika sekta ya kilimo. Hapo kesho, rais Kenyatta ataelekea nchini Uganda kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais Yoweri Museveni. Ndege aliyosafiria rais Kenyatta na mama taifa, Margaret Kenyatta iliondoka kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta muda mfupi baada ya saa tatu leo asubuhi.