Rais Uhuru asema hakuna pengo lolote la uongozi humu nchini

Rais Uhuru Kenyatta  amesema kwamba hakuna pengo lolote la uongozi humu nchini kwa vile serikali iliyo mamlakani ilichaguliwa ki-halali.  Akihutubu wakati wa sherehe rasmi za ufunguzi wa Bunge, Rais  Kenyatta alionya kwamba hatavumilia matendo yoyote ya ghasia wakati huu ambapo wakenya wanajiandaa kwa marudio ya uchaguzi wa Urais tarehe 17 Oktoba kufuatia uamuzi wa mahakama ya juu. Alihimiza Bunge kusimama imara kwa minajili ya katiba na kulinda haki ya Wakenya kujiamulia mambo yao. Rais alisema kwamba Wa-Bunge wana jukumu la kuchunguza asasi nyingine za serikali wakati wowote zinapoingilia uhuru wa wakenya. Rais alisema ni muhimu kwa asasi zote za serikali kuwa huru kutokana na aina yoyote ya unyanyasaji  wala kuelegezwa na wadau wa kigeni ama wa humu nchini, na pia makundi yenye maslahi maalum. Alisema nchi hii inakabiliwa na nyakati ngumu na hivyo kuna haja kwa kila mojawapo ya asasi tatu za serikali kuheshimu uhuru wa asasi nyingine. Rais alipongeza pia idadi inayozidi kuongezeka ya wanawake waliochaguliwa bungeni na pia mtindo wa wakenya kuwachagua vijana kuwa waakilishi wao bungeni. Rais Kenyatta aliwakumbusha wakenya  kwamba mashindano ya uchaguzi sio kinyang’anyiro baina ya watu wawili bali fursa kwa wakenya kudhihirisha haki yao ya kuwachagua viongozi.