Rais Uhuru Amtaka Jaji Mkuu Kuwahukumu Wafisadi Wakuu

Rais Uhuru Kenyatta anamtaka jaji mkuu mpya David Maraga kuhakikisha kesi za ufisadi ambazo zingali mahakamani zinashughulikiwa haraka. Rais hasa anataka kesi za ufisadi zinazowahusu baadhi ya watu wenye nyadhifa za juu katika jamii kusikizwa na kuamuliwa haraka ili kurejesha imani ya umma kwenye vita dhidi ya uovu huo. Akiongea huko Machakos alipoliongoza taifa kuadhimisha siku kuu ya saba ya siku ya Mashujaa chini ya katiba ya sasa, kiongozi wa nchi alisema aliamua kuwaachilia huru wafungwa 7000 wenye makosa madogo madogo ili kubuni nafasi zaidi gerezani kuwahukumu wale wanaohusika na hatia za ufisadi.

Wakati wa mkutano kuhusu uongozi na utawala katika ikulu ya Nairobi siku ya Jumanne, rais KenyattaA� alishtumu baadhi ya taasisi zilizo na mamlaka ya kukabiliana na ufisadi ikiwa ni pamoja na tume ya maadili na vita dhidi ya ufisadi, ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma na idara ya mahakama kuhusu kucheleweshwa kukamilishwa kesi zilizowahusu waliokuwa maafisa wakuu serikalini ambao aliwasimamisha kazi kuhusiana na madai ya ufisadi. Alisema baadhi ya wale aliowafuta kazi sasa wanafanya kampeni dhidi ya kuchaguliwa kwake kwa kipindi kingine kwenye uchaguzi mkuu mwaka ujao.