Uhuru ashutumu upinzani kwa kutishia kususia kikao cha kufungua bunge

Rais Uhuru Kenyatta amewashtumu wapinzani kuhusiana na tishio lao la kususia kikao cha ufunguzi rasmi wa bunge leo. Rais alisema kuwa tishio hilo halina maana yoyote kwani chama cha Jubilee kina idadi ya kutosha ya wabunge kutekeleza shughuli bungeni. Chama cha Jubilee na vyama vyake tanzu vina wabunge 213 kati ya 349 bungeni. Rais ambaye aliandamana na naibu rais William Ruto aliyasema haya katika ikulu ya Nairobi, alipokutana na viongozi wa eneo la Ukambani wakiongozwa na gavana wa Machakos Dr Alfred Mutua, gavana wa Nairobi Mike Sonko na wabunge watatu wa chama cha Jubilee kutoka eneo hilo.A�Rais pia alikutana na baraza la wazee wa jamii ya Bukusu waliosema watawashawishi wapigaji kura kumchagua rais kwenye marudio ya uchaguzi. Wazee hao wakiongozwa na mwenyekiti wao Richard Walukano walisema kuwa jamii ya Bukusu imenufaika pakubwa kutokana na miradi iliyotekelezwa na rais Kenyatta na hivyo watamuunga mkono.A�Walisema watatekeleza kampeni za nyumba hadi nyumba katika kaunti za Bungoma, Busia, Kakamega na Trans Nzoia kuhakikisha kwamba rais Kenyatta atapata kura nyingi kutoka kwenye eneo hilo kuliko alizopata tarehe 8 mwezi uliopita.