Rais Kenyatta kuzuru kaunti tano wiki hii

Rais Uhuru Kenyatta atazuru kaunti za Pokot magharibi, Bungoma, Uasin Gishu, Nakuru na Nairobi. Atatumia ziara hizo katika kaunti hizo kuwashukuru wakazi kwa kudumisha amani na kuwapigia kura viongozi wa chama cha Jubilee kuanzia wabunge wa kaunti hadi rais wakati wa uchaguzi mkuu hapo Agosti 8. Pia atatumia ziara hizo kuwaandaa wakazi kujitokeza kwa wingi na kwa mara nyingine tena kumpigia kura kwakuwa tarehe ya uchaguzi mpya wa urais imetangazwa. Rais Kenyatta ataanza ziara yake kesho kwa kuzuru Chepareria, Pokot magharibi na Bungoma kabla ya kwenda hadi Eldoret. Siku ya Ijumaa Rais atapeleka kampeini zake katika kaunti za Kericho na Nakuru ambako atahutubia wakazi huko Kapkatet na Naivasha mtawalia. Atakamilisha duru ya kwanza ya kampeini yake Jumamosi kwa kufanya ziara ya kukutana na wananchi katika kaunti ya Nairobi ambako atasisitiza ujumbe wa amani na haja kwa wakazi kujitokeza kwa wingi kutekeleza haki yao ya kikatiba hapo Oktoba 17 katika uchaguzi mpya wa urais kama walivyofanya hapo Agosti 8.