Rais Kenyatta azindua uwanja wa ndege wa kimataifa wa Isiolo

Rais Uhuru Kenyatta amezindua ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Isiolo kwa gharama ya shilingi bilioni 2.5 ambao ni sehemu ya mradi wa uchukuzi wa LAPPSET kutoka bandari ya Lamu kupitia Sudan kusini hadi Ethiopia. Uwanja huo wa ndege umo katika sehemu bora kwa usafirishaji, miraa, nyama ya nga��ombe na mazao mabichi kutoka nyanda za chini za eneo la masahariki. Akiongea wakati wa halfa hiyo, rais Kenyatta, alisema uwanja huo wa ndege pia utafungua eneo la utalii la kaskazini mwa nchi ili kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha uchumi kwa manufaa ya wakazi. Alisema uwanja huo wa ndege utaimarisha vivutio vya utalii kaskazini mwa nchi ambavyo ni pamoja na utalii kuhusu mandhari ya mazingira, utamaduni, hifadhi za kitaifa, mashamba ya kibinafsi, hifadhi za wanyama pori na mji wa utalii unaotarajiwa kujengwa katika sehemu hiyo. Uwanja huo wa ndege wa kisasa, ambao uko katika kaunti ya Isiolo huku nusu ya barabara yake ya kupaa ndege ikiwa katika kaunti ya Meru umejengwa katika eneo la hekari 329.76 na uko futi 3,501 juu ya eneo la bahari. Uwanja huo wa ndege unaweza kuwahudumia abiria elfu-125 kila mwaka huku ukiwa na eneo la kuegesha magari 200. Rais Kenyatta aliandamana na naibu rais William Ruto na viongozi wengine wa Jubilee.