Rais Kenyatta awashauri Wakenya kudumisha amani

Rais Uhuru Kenyatta amewahimiza Wakenya kudumisha amani na kukataa vishawishi vya kuzua ghasia. Akiongea kwenye hafla ya kuapishwa kwa gavana mpya wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko na naibu wake, Polycarp Igathe katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, rais Kenyatta aliwarai Wakenya kuombea amani na umoja hapa nchini. Rais Kenyatta aliwapongeza Sonko na naibu wake, Igathe kwa ushindi wao na kuwahakikishia kuwa serikali ya kitaifa itashirikiana na ile ya kaunti ya Nairobi kuboresha jiji la Nairobi kwa manufaa ya wakazi na Wakenya wote. Aidha rais alimpongeza gavana anayeondoka, Evans Kidero kwa kukubali kushindwa na kumpokeza mamlaka gavana Sonko akisema hiyo ni ishara ya siasa komavu na uzalendo. Magavana-31 wanaapishwa leo.