Rais Kenyatta ataka uajibikaji katika matumizi ya pesa za umma

Rais Uhuru Kenyatta amewataka wale wote waliopewa jukumu la kusimamia pesa za umma kuhakikisha zinatumiwa kwa uadilifu na kwa sababu zilizonuiwa. Akiongea jana alipofungua rasmi maonyesho ya kimataifa ya mwaka huu ya kilimo kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Nairobi, rais hasa alitahadharisha halmashauri ya kitaifa ya nafaka na mazao, NCPB, dhidi ya utumiaji mbaya wa pesa za umma kwa kuwalipa wafanyibiashara walaghai badala ya kuwalipa wakulima wa mahindi.

Alisema kuwa wakulima wa mahindi wanaoidai halmashauri hiyo shilingi bilioni-1.4 na ambao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo tayari wameanza kupokea malipo yao kutoka NCPB.

Uhuru pia aliwaagiza wasagaji mahindi kupunguza bei ya pakitti ya kilo mbili ya unga wa mahindi hadi shilingi 75. Alisema kuwa mwaka huu nchi hii itakuwa na hifadhi ya magunia milioni-56 ya mahindi ilhali magunia milioni- 52 hutumika kwa mwaka na hivyo ipo haja ya kupunguza bei hiyo.

Wakati huo huo Rais Kenyatta alisema kwua serikali inatetea utumiaji wa unga wa mahindi uliochanganywa na ule wa aina nyingine za mimea ili kuhimiza uzalishaji wa mime ainayohimili ukame ukiwemo mtama.

Alisema ni fahari kwa nchi hii kuongoza katika sayansi na ubunifu barani Afrika. Maudhui ya maonyesho ya mwaka huu ni kuimarisha teknolojia na ubunifu katika kilimo ili kuafikia ajenda nne kuu za maendeleo nchini.