Rais Kenyatta aongoza taifa kwenye maridhiano

Rais Uhuru Kenyatta leo aliwaongoza viongozi wa kisiasa na kidini kwenye maridhiano wakati wa hafla ya mwaka huu ya maombi ya kitaifa jijini Nairobi. Akiwahimiza Wakenya na viongozi kusameheana, rais aliwaleta pamoja viongozi wa upinzani Raila Odinga na Kalonzo Musyoka ambao walisalimiana na naibu rais William Ruto. Viongozi hao wanne walisimama pamoja kama ishara ya umoja na kusameheana kufuatia uchaguzi mkuu uliozua mihemko ya kisiasa mwaka uliopita.

Rais alisema kwenye maongozi ya demokrasia, tofauti sharti zichipuze lakini akatahadharisha kwamba tofauti hizo hazipaswi kuwagawanya Wakenya. Alisema  maongozi ya demokrasia hayapaswi kusababisha migawanyiko na uharibifu wa mali. Alisema kile Wakenya wanataka ni nyumba bora, huduma bora za afya na kawi ya kuimarisha sekta ya utengenezaji bidhaa.

Rais aliwaonya wale wanaojihusisha kwenye ufisadi akisema hawatafaulu hata wakijaribu kujificha nyuma ya jamii za makabila yao.