Rais Kenyatta aomboleza Nkaissery

Kufuatia kifo cha waziri wa usalama wa kitaifa meja Jenerali Joseph Nkaissery, rais Uhuru Kenyatta kwa niaba ya serikali, ametuma risala za rambi rambi kwa familia, marafiki na jamaa za marehemu pamoja na jamii ya wamaasai. Akihutubia taifa kutoka ikulu ya Nairobi, rais alimtajaA�A�A�A� Nkaissery kuwa kiongozi mashuhuri huku akiwahimiza Wakenya waomboleze kwa amani. Aidha aliwahimiza wakenya wawe watulivu huku wakisubiri uchunguzi wa maiti kubaini kilichosababisha kifo chake.

Akikitaja kisa hicho kuwa cha kuhuzunisha, rais aliwahakikishia wakenya kwamba usalama wa nchi hii umedumishwa na kwamba wadau wote wataendelea kutekeleza majukumu yao kama inavyotakiwa.

Wakati uo huo, rais Uhuru Kenyatta amefutilia mbali mkutano wa chama cha Jubilee uliotarajiwa kufanywa leo katika kaunti ya Turkana. Rais na naibu wake badala yake wataungana na familia ya marehemu Nkaissery katika kuomboleza waziri huyo. Viongozi hao wawili wa chama cha Jubilee walitarajiwa kufanya kampeni katika maeneo ya Lokitaung, Kakuma, Lodwar na Lokichar katika kaunti ya Turkana. Ikulu ya rais haijasema ni lini rais atafanya kampeni yake huko Turkana baada ya kufutilia mbali ziara hiyo iliyotarajiwa kufanywa leo.