Rais Kenyatta Akitaka Chama Cha Mchezo Wa Gofu Kuwahusisha Wakenya Zaidi

Rais Uhuru Kenyatta amekitaka chama cha mchezo wa gofu hapa nchini kuhakikisha wakenya zaidi wanashiriki kwenye mchezo huo. Alisema serikali itaendelea kushirikiana na chama cha gofu kuwahusisha wakenya zaidi kwenye mchezo huo ambao umeanza kupata umaarufu hapa nchini. Rais Kenyatta alisema hayo jana katika uwanja wa gofu wa Karen jijini Nairobi ambako alikuwa mgeni wa heshima wakati wa kumalizika kwa mchuano wa gofu uliodhaminiwa na benki ya Barclays na kuwatuza washindi. Rais Kenyatta alidokeza kuwa serikali itatoa ardhi zaidi kwa chama cha gofu katika uwanja wa michezo wa Kasarani ili kujenga ukumbi wa pili wa gofu kwa umma. Ukumbi wa kwanza wa gofu kwa umma umejengwa katika bustani ya Jamhuri jijini Nairobi. Waziri wa michezo, utamaduni na sanaa, Dr Hassan Wario alitoa wito kwa vijana kuthamini michezo kwani inaleta tija.