Rais Kenyatta ahimiza Raila kuabudu amani

Rais Uhuru Kenyatta ametoa wito kwa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kuwaelezea wakenya sera zake badala ya kutoa taarifa ambazo huenda zikazua ghasia. Rais alisema ni jambo la kusikitisha kwamba kiongozi huyo wa upinzani anaendelea kutoa taarifa kama hizo badala ya kuabudu amani. Akihutubia wakazi wa kaunti ya Embu, rais Kenyatta alitaja madai ya upinzani kwamba serikali inapania kutumia wanajeshi kuzua ghasia kuwa yasiyo na msingi wowote. Wakati huo huo, rais Kenyatta aliyekuwa ameandamana na naibu wake William Ruto aliwataka wakazi wa sehemu hiyo kuhakikisha kuwa kila mmoja wao anashiriki kwenye uchaguzi ujao na kuunga mkono chama cha Jubilee. Naibu rais aliwataka wakazi wa Embu kujitokeza kwa wingi na kupigia kura Jubilee kwenye uchaguzi mkuu ujao wa tarehe nane mwezi Agosti kwa vile chama hicho kimejitolea kubadili maisha ya wakenya wote. Aliwataka kukatalia mbali jaribio la upinzani la kutatiza miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa. Rais na naibu wake baadaye walihutubia wananchi huko Tala kaunti ya Machakos ambapo waliwarai kuwaunga mkono kwenye uchaguzi.