Rais Kenyatta ahakikishia wakenya usalama wao

Rais Uhuru Kenyatta amesema serikali itaimarisha usalama humu nchini na kwamba shughuli zitaendelea kama kawaida hata baada ya kifo cha waziri wa Usalama wa taifa Meja jenerali mustaafu Joseph Nkaissery. Akiongea katika kaunti ya Baringo Rais alisema vikosi vya usalama vitaimarisha hatua za kuwalinda wakenya katika kumkumbuka marehemu waziri. Alionya kuwa wale wanaodhani kuwa wanaweza kupata nafasi ya kuwadhuru wakenya kwamba watafanya kosa kubwa. Kiongozi wa taifa alikuwa akihutubu alipokutana na wananchi kwenye ziara yake huko Kabartonjo na Marigat, katika kaunti ya Baringo akiandamana na naibu wa rais William Ruto. Jenerali Nkaissery ambaye alifariki siku ya Jumamosi aliongoza moyo wa marekebisho na bidii katika vikosi vya usalama na alipongezwa kwa kudumisha imani katika sekta hiyo. Awali Rais Kenyatta na naibu wake walikuwa miongoni mwa maelfu ya waumini wa kikristo waliohudhuria ibada ya jumapili katika kanisa la AIC Kabortonjo katika kaunti ya Baringo.