Rais Kenyatta aahirisha ziara yake eneo la magharibi mwa nchi

Rais Uhuru Kenyatta ameahirisha ziara yake katika eneo la magharibi mwa nchi. Kwenye taarifa kwa vyumba vya habari, hatibu wa Ikulu, Manoah Esipisu, alisema rais aliahirisha ziara hiyo ili kutoa fursa kwa vyama vya kisiasa kuwasilisha orodha zao za uteuzi wa wawaniaji nyadhifa za uchaguzi kwa tume ya uchaguzi kwani hii ndio wiki ya mwisho ya kutekeleza shughuli hiyo. Alisema rais amemakinika kuhakikisha shughuli zote zinatimizwa kama inavyohitajika na mwongozo uliotolewa na asasi zilizojukumiwa kuhakikisha shughuli ya uteuzi inafanywa kwa njia ya uadilifu. Ziara ya rais Kenyatta katika kaunti za Tharaka Nithi na Meru pia iliahirishwa kutokana na sababu sawia na hizo. Esipisu alisema tarehe ya ziara hizo itatangazwa baadaye.