Rais Castro Na Obama Watofautiana Kuhusu Haki Za Kibinadamu

Rais Raul Castro wa Cuba na mwenzake wa Marekani, Barack Obama walitofautiana kuhusu swala la haki za binadamu hususan gereza la Marekani lililoko Guantanamo Bay na wafungwa wa kisiasa wa Cuba. Kwenye mkutano wao wa kihistoria, Castro alisema kama angelipewa orodha ya wafungwa wa kisiasa, angeliwaachilia huru mara moja. Awali, ikulu ya White House ilisema imekabidhi Cuba orodha ya waasi kutoka nchi hiyo lakini Cuba haiwachukulii waasi hao kuwa wafungwa wa kisiasa, swala ambalo limekuwa kizingiti kwenye juhudi za kutatua mzozo kati ya nchi hizo mbili. Alisema hatua zaidi zinahitajika ili kuondoa vikwazo vilivyowekwa Cuba huku akiongeza kuwa gereza la Guantanamo Bay sharti lifungwe. Obama alisema vikwazo vya kibiashara dhidi ya Cuba vitaondolewa na kwamba hatima ya raia wa Cuba itaamuliwa na wao wenyewe na sio nchi nyingine.