Rais Barack Obama Ataja Shambulizi La Jana Kuwa Kitendo Cha Ugaidi Na Chuki

Rais Barack Obama wa Marekani ametaja shambulizi la jana katika kilabu kimoja cha Orlando huko Florida kuwa kitendo cha ugaidi na chuki. Rais Obama alisema wamerikani wameungana wakati huu wa majonzi kufuatia mkasa huo. Katika shambulizi hilo mwanaume mmoja mwenye umri wa miaka  29 kwa jina Omar Mateen aliwaua kwa kuwapiga risasi watu  50 na kuwajeruhi  wengine  53 katika kilabu cha  Pulse kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi na polisi.

Kundi la Islamic State limedai kuhusika na shambulizi hilo. Rais Obama ambaye alishinikiza pakubwa kuwepo kwa sheria kali zaidi za umiliki wa silaha, alisema mauaji ya kikatili ya watu wasio na hatia ni dhihirisho la namna ilivyo rahisi kupata silaha hatari nchini Marekani.