Rais Awapongeza Washika Dau Wa Elimu

Rais Uhuru Kenyatta amewasifu maafisa wa wizara ya elimu na mashirika husika kwa kuhakikisha kwamba matokeo ya mitihani ya kitaifa ya mwaka huu ni ya kuaminika. Rais Kenyatta alisema mpango wa serikali wa marekebisho yanayolenga kuhakikisha matokeo ya mitihani ya kitaifa ni ya kuaminika unatekelezwa. Rais Kenyatta aliwahakikishia watahiniwa wote wa mtihani wa mwaka huu kuwa licha ya matokeo yoyote watakayopata, bado kuna matumaini ya kuhitimu taaluma zao. Alisema hata ingawa matokeo ya mwaka huu yalikuwa ya kiwango cha chini ikilinganishwa na mwaka jana, hali ya kawaida ilishuhudiwa katika hatua zote za mtihani huo, ishara kuwa ulifanyika na kusahihishwa kwa njia inayofaa. Rais pia aliiagiza wizara ya elimu kuweka mikakati dhabiti ili kuhakikisha mageuzi yote yanayoendelea katika sekta ya elimu hapa nchini ni ya kudumu. Alisema hatua mahususi zitachukuliwa ili kuhakikisha kuwa wizara ya elimu inatumia ipasavyo pesa zinazotengewa na serikali na kukomesha ufisadi ambao unahujumu utekelezaji wa malengo yaliyowekwa.