Raila Odinga Awatahadharisha Polisi Dhidi Ya Kutumiwa Kama Chombo Cha Kukabiliana Na Upinzani

Kiongozi wa CORD Raila Odinga amewatahadharisha polisi dhidi ya kutumiwa kama chombo cha kukabiliana na upinzani. Akiongea wakati wa hafla ya maombi ya kutoa shukurani ya mwakilishi wa wanawake katika kaunti ya Busia Florence Mutua katika chuo anuai cha Butula kaunti ya Busia , Raila alisema polisi wanafaa kukataa kutumiwa kuwahangaisha watu wasio na hatia na viongozi wanaotetea haki zao na zile za raia. Raila alitoa wito kwa polisi wa hapa nchini kuiga mfano wa wenzao wa Tanzania na Uingereza ambao ni marafiki na wananchi. Matamshi yake yamejiri siku chache baada ya wanasiasa wanane kuzuiliwa korokoroni na baadaye kuachiliwa huru kwa madai ya kutoa matamshi ya chuki. Akiongea katika hafla hiyo seneta wa kaunti ya Machakos Johnstone Muthama ambaye alikuwa mmoja wa wale waliozuiliwa ,alitoa wito kwa serikali ya Jubilee kukomesha ubaguzi katika vita dhidi ya uenezaji matamshi ya chuki na uchochezi. Kwa upande wake mbunge wa Suna Mashariki Junnet Mohammed alipuzilia mbali madai ya naibu rais William Ruto kuwa wale wanaoshirikiana na Raila ni watumwa. Akizungumzia mzozo uliozuka hivi majuzi katika chama cha ODM kutokana na hali ya katibu mkuu wa chama hicho Ababu Namwamba kuhusishwa na muungano wa Jubilee, Ruto wiki iliyopita aliwataka wakenya kutokubali kuwa watumwa wa vyama fulani vya kisiasa, bali wafanye maamuzi ya busara kabla ya uchaguzi mkuu ujao.