Raila atetea ushirikiano wake na Rais Kenyatta

Miito ya umoja ilisheheni kwenye ulingo wa siasa mwishoni mwa wiki hii huku kiongozi wa upinzani Raila Odinga akiwakosoa wale wanaoshtumu uamuzi wake wa kukutana na hatimaye kufanya kazi na rais Uhuru Kenyatta. Raila amesema hatua hiyo imeokoa nchi hii kutokana na zogo la kisiasa, akisisitiza haja iliyopo ya kudumisha umoja.

Akiongea wakati wa ibada ya kanisa katika mtaa wa Maringo jijini Nairobi. Kiongozi huyo wa upinzani aliwapuuzilia mbali wale wanaomshtumu wakidai eti anajitakia makuu. Alisema nchi hii ni muhimu zaidi kuliko watu binafsi ama vyama vya kisiasa na hivyo basi ipo haja ya kukuza maridhiano licha ya miegemeo ya kisiasa. Kiongozi huyo wa chama cha ODM ambaye aliandamana na wanasiasa kadhaa kutoka Nairobi aliwahimiza Wakenya kuzingatia umoja akisema migawanyiko ya kisiasa itaathiri taifa hili.  Alihimiza serikali kuzingatia mshikamano wa kitaifa kwa kuhakikisha ugavi sawa wa rasilimali za kitaifa.

Wakati huo huo wabunge James Gakuyu wa Embakasi kaskazini, Charles Njagua wa Starehe, Kimani Ichung’wah wa Kikuyu na gavana wa Taita Taveta Granton Samboja wamewapuuzilia mbali wale wanaoeneza siasa za  migawanyiko, wakisema kuna umoja zaidi baada ya viongozi hao wawili kuafikiana. Katika kaunti ya Kiambu naibu mwenyekiti wa chama cha Jubilee, David Murathe, na mbunge wa Kiambu Jude Jomo waliwahimiza Wakenya kujiepusha na jaribio lolote la kuwagawanya kwa msingi ya kisiasa.