Raila arejea Kenya baada ya kuzuru Ulaya

Kiongozi wa muungano wa NASA Raila Odinga amerejea nchini. Raila alilakiwa na mamia ya wafuasi na wabunge wa upinzani waliozingirwa na polisi kumkaribisha.Msafara wa viongozi wa upinzani ulipitia barabara ya Mombasa huku kukiripotiwa ghasia katika baadhi ya sehemu walikopitia. Awali maafisa wa polisi walilazimika kufyatua risasi hewani na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi waliokuwa wakielekea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta kumlaki kiongozi huyo wa upinzani A�aliyerejea nchini kutoka Marekani. Eneo la mzunguko wa barabara wa City Cabanas halikuruhusiwa watu huku waandamanaji wakiwasha moto barabarani. A�Wale waliokuwa wakielekea katika uwanja wa ndege walitakiwa kutoa stakabadhi za uthibitisho kuwa wanasafiri ili waruhusiwe huku wengine wakikatazwa kupita. Inspekta Jenerali wa polisi Joseph Boinnet mapema wiki hii alionya kwamba wafuasi wa NASA waliopanga kumlaki Odinga hawataruhusiwa kuingia katika uwanja wa ndege wa Jomo kenyatta. Kwingineko katika barabara ya Jogoo wafuasi hawakuweza kufika katika uwanja wa ndege kutokana na kuwepo kwa polisi wengi na wakawasha moto barabarani kutatiza usafiri katika barabara hiyo yenye shughuli nyingi. Viongozi wa NASA wanatarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara katika bustani ya Uhuru.