Raila aelezea matumaini kushinda kesi yake mahakamani

Kiongozi wa muungano wa NASA- Raila Odinga ameelezea matumaini yake ya kushinda katika kesi aliyo-wasilisha katika Mahakama ya juu kupinga uchaguzi wa Rais Uhuru Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu tarehe 8 mwezi Augosti. Raila amesema kuna kila sababu ya kuamini ushahidi utakaowasilishwa na upinzani mbele ya Ma-jaji saba wa mahakama ya juu, unatosha kwa mahakama kukubaliana na hoja zake.

Akiongea jana baada ya kuhudhuria Ibada ya Jumapili kwenye kanisa la All Saints Cathedral Jijini Nairobi, kiongozi huyo wa NASA aliyeandana na vinara wenza, Kalonzo Musyoka na Seneta wa Bungoma, Moses Wetangula, alisema azma ya upinzani kushika hatamu za uongozi wa taifaA� ingalipo.

Wakati huo huo, Polisi hapo jana walikatalia mbali ombi la muungano wa upinzani, NASA kuandaa maombi nje ya mahakama ya juu. Kamanda wa Polisi Jijini Nairobi, Japheth Koome alisema jambo hilo halitawezekana, kutokana na sababu za kiusalama.

Polisi waliimarisha usalama nje ya Jumba la mahakama ya Juu na pia katika maeneo yaliyo karibu, huku Ma-jaji saba wakipanga kusikiza kesi iliyowasilishwa na muungano wa NASA, kupinga matokeo ya uchaguzi wa Urais kuanzia saa tatu asubuhi hivio leo.