Raila aapa hataomba msamaha kuhusiana na matamshi yake

Kiongozi wa upinzani Raila Odinga amesema hawezi kuomba msamaha kwa matamshi aliyotoa alipokuwa akifanya kampeini huko Kajiado siku ya Alhamisi alipoihimiza jamii ya wamaasai kutouza ardhi ya mababu zao. Katika taarifa,A� Odinga alitetea matamshi yake akisema kuwa ardhi hiyo ilipotea kutokana na dhuluma za kihistoria kama ilivyoandikwa katika taarifa ya tume ya Ukweli, haki na maridhiano ambayo mapendekezo yake hayajatekelezwa. Kinara huyo mkuu wa upinzani anashutumiwa kwa kueneza matamshi ya chuki. Katibu mkuu wa chama cha ODM Agnes Zani alisema kwamba matamshi ya Odinga yalitolewa ili kuwapa uwezo wa kijamii na kiuchumi jamii hiyo. Seneta maalum Elizabeth Ongoro pia alimtetea kiongozi wa chama chake cha zamani ambaye pia ni mgombea urais na akakishutumu chama kinachotawala kwa kutafuta kujisafisha kwa matamshi yake ya kiholela kwa kutaka kumsulubisha Odinga. Matamshi ya Odinga si ya pekee yaliyovutia shutuma kali. Kiongozi wa walio wengi katika bunge la taifa Adan Duale ambaye alitoa wito wa kukamatwa kwa Odinga hivi karibuni alishutumiwa kwa madai ya kuwachochea wananchi katika eneo bunge lake kufukuza jamii moja kutoka kaunti ya Garissa. Hapo jana rais Uhuru Kenyatta aliushutumu upinzani kwa kutumia mbinu ya kuwagawanya wananchi katika hatua ya kuungwa mkono kisiasa.