Raia Wa Djibouti Kupiga Kura Kumchagua Rais Mpya

Shughuli ya upigaji kura kwenye uchaguzi wa urais nchini Djibouti imeanza ambako rais Ismail Omar Guelleh anawania kipindi cha nne uongozini dhidi ya upinzani dhaifu. Guelleh amekuwa mamlakani tangu mwaka 1999 na amekosolewa kwa kushikilia mamlaka. Anakabiliana na wapinzani watano lakini upinzani unalalamika kuhusu ukatili wa maafisa wa polisi na vyombo vya habari kuegemea upande mmoja. Shughuli hiyo ilianza leo asubuhi ingawa ilinza taratibu huku wapigaji kura wachache mno kati ya elfu-180 wakijitokeza mapema. Matokeo ya uchaguzi huo huenda yakajulikana leo jioni. Wapinzani wamekasirika kwamba rais huyo alibatilisha uamuzi wake wa awali wa kutowania kipindi cha nne. Mpinzani wake mkuu anayeakilisha chama cha upinzani cha Union for National Salvation (USN) ni Omar Elmi Kaireh, ambaye ni shukaa wa uhuru wa nchi hiyo. Hata hivyo mwaniaji mwingine Mohamed Daoud Chehem, wa kundi lililojitenga kutoka kwa chama cha USN amezungumzia kuhusu kugawika kwa upinzani. Baadhi ya vyama vingine vya upinzani vinasusia uchaguzi huo.