Raia wa China aliyetoa matamshi ya ubaguzi arejeshwa kwao

 Raia mmoja wa China ambaye alirekodiwa kwenye video  akitoa matamshi ya  ubaguzi wa rangi dhidi ya  Wakenya  amerejeshwa nchini mwao. Liu Jiaqi alikamatwa jana usiku  na maafisa wa usalama  baada ya idara ya uhamiaji kufutilia mbali leseni yake ya kufanya kazi hapa nchini.

Akithibitishwa kukamatwa na kurejesha nchini  China kwa Liu,  Katibu wa  Uhamiaji Meja Mstaafu Gordon Kihalangwa aliliambia  shirika la Habari Nchini, KBC,  kwa  njia ya simu kuwa  Liu Jiaqi aliondoka hapa nchini leo saa tano unusu  asubuhi.

Raia  huyo wa China alianswa  kwenye video hapo jana akitumia matamshi chafu  dhidi ya Wakenya na viongozi wake.  Kwenye kanda hiyo iliyosambazwa, mwanamume huyo  anasikikika akitumia matamshi ya kejeli dhidi ya Wakenya.  Tukio hilo liliwakera Wakenya  ambao walitaka akamatwe na kutimuliwa nchini.