Raia Wa Afghanistan Warejeshwa Kwao

Raia 38 wa Afghanistan wamewasili jijini Kabul kutoka ujerumani hili likiwa kundi la kwanza kurejeshwa nchini humo kufuatia mkataba ulioafikiwa baina ya nchi hizo mbili mwaka huu baada ya maombi yao ya kutafuta hifadhi kukataliwa.Ndege ya kukodishwa iliyowabeba raia hao ambao wote ni wanaume iliwasili kwenye jiji hilo kuu la Afghanistan kutoka Frankfurt. Ndege nyingine inayobeba kundi jingine itawasili humo mapema mwezi Januari kwa mujibu wa vyombo vya A�habari nchini ujerumani. Msemaji mmoja amesema kuwa wizara ya kuwashughulikia wakimbizi nchini Afghanistan itawasaidia watu hao kurejea kwenye makazi yao akiongeza kusema kuwa takriban raia elfi-10 wa Afghanistan wamerejeshwa nchini mwao kutoka barani ulaya mwaka huu. Shughuli hiyo inatekelezwa chini ya mkataba ulioafikiwa baina ya ujerumani na Afghanistan mwezi Oktoba, lakini mkataba huo ulizua maandamano nchini ujerumani huku wakosoaji wakisema kuwa maeneo mengine nchini Afghanistan sio salama na kwamba huenda watu wanaorejeshwa wakakumbwa na hali ngumu.