Raia mmoja wa Vietnam akamatwa katika JKIA na maafisa wa huduma kwa wanyama pori.

Raia mmoja wa Vietnam alikamatwa jana asubuhi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta-JKIA akiwa na meno nane na kucha tatu za simba, na meno mbili za ngiri. Mshukiwa alikamatwa na maafisa wa shirika la huduma kwa wanyama pori.

Bidhaa hizo za wanyama pori zilipatikana zimefichwa ndani ya chupa-chai zikiwa zimefungwa kwa karatasi. Kulingana na taarifa kutoka afisi ya mawasiliano ya shirika la KWS, mshukiwa huyo kwa jina Truong Trung Hieu alikuwa akisafiri kutoka Liberia kuelekea Bangkok kupitia Kenya.

Amezuiliwa katika kituo cha polisi cha JKIA na atafikishwa mahakamani leo mkalimani akipatikana. Kukamatwa kwake kumejiri muda mfupi baada ya mkutano kuhusu biashara haramu ya bidhaa za wanyama pori kumalizika mjini London, ambako mkewe rais wa Kenya Margaret Kenyatta aliongoza ujumbe wa Kenya katika kutoa wito wa kuimarishwa kwa ukaguzi katika vituo vyote vya kuingia na kuondoka nchini ili kuhakikisha walanguzi wa bidhaa za wanyama pori wamenaswa.