Prof Magoha abuni kamati kutathmini uwezekano wa kufunguliwa tena kwa shule

Kamati ya watu kumi imebuniwa na Wizara ya Elimu kutathmini uwezekano wa kufunguliwa tena kwa shule nchini.

Waziri wa Elimu Prof. George Magoha, alizindua kamati hiyo Jumanne, ambayo itaongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Ustawi wa Mtaala Nchini Dr. Sarah Ruto.

Wanachama wengine wa kamati hiyo ni pamoja na Indimuli Kahi Mwenyekiti wa  Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Upili, Nicholas Gathemia, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Msingi, Peter Ndoro Afisa Mkuu wa Chama cha Shule za Kibinafsi Nchini, Jane Mwangi wa Chama cha Shule Huru za Kimataifa Nchini, Peter Sitienei Mwenyekiti wa Walimu Wakuu wa Shule za Watu Wenye Ulemavu pamoja na Waakilishi wa Wazazi na Makundi ya Kidini.

Kwenye taarifa Prof. Magoha alisema kamati hiyo itamshauri kuhusu kufunguliwa tena kwa shule za msingi,zile za upili, vyuo vya walimu na taasisi za elimu ya watu wazima.

Kuchunguza upya kalenda ya shule kama sehemu ya juhudi za kujinusuru kutokana na chamko la COVID-19. Kutoa mapendekezo ya kukabiliana na majanga katika siku za usoni na kumshauri waziri kuhusu athari za chamko la Covid 19 kuhusiana na elimu.

Aidha kamati hiyo itamshauri waziri kuhusu hatua za kiafya na usalama zitakazochukuliwa kuwalinda wanafunzi, walimu na wahudumu wengine wa shule.

Serikali iliahirisha kufunguliwa kwa shule kwa muda wa mwezi mmoja  ili kutoa fursa ya kukabili maradhi ya Covid-19 ambayo yamesambaratisha shughuli sio tu humu nchini bai pia ulimwengu mzima kwa jumla.