Prof Kobia ataka magavana kutowafuta wafanyikazi kiholela

Mwenyekiti wa tume ya kuajiri watumishi wa umma, Profesa Margaret Kobia ametahadharisha serikali za kaunti dhidi ya kuwaachisha kazi kiholela wafanyikazi wa serikali za kaunti akisema hatua hiyo huenda ikagharimu kiasi kikubwa cha pesa. Profesa Kobia alionya kuwa pesa za umma hazitatumiwa kugharamia kesi za wafanyikazi waliotimuliwa bila kuzingatia utaratibu unaofaa. Profesa Kobia alisema wafanyikazi wote kwenye kaunti wakiwemo wale walioajiriwa kwa kandarasi wanafanya kazi kuambatana na katiba na sheria za ajira ambazo lazima zizingatiwe kikamilifu. Tahadhari ya Prof Kobia imejiri kufuatia vitisho vya baadhi ya magavana waliochaguliwa hivi majuzi vya kuwatimua watumishi wa umma kwenye kaunti zao kwa sababu mbalimbali ikiwemo kuwaunga mkono wapinzani wao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mapema mwezi huu. Tayari baadhi ya magavana wamewasimamisha kazi baadhi ya wafanyikazi wa serikali za kaunti kwa sababu zinazoonekana kuwa za kisiasa.A�