Polisi Tanzania wasaka watekaji nyara wa bwanyenye, Mohammed Dewji

Polisi nchini Tanzania wanawasaka watekaji nyara wa bwanyenye, Mohammed Dewji. Dewji al-maarufu ‘Mo’ alitekwa nyara mapema leo alipokuwa akielekea katika mkahawa wa Colosseum kufanya mazoezi ya viungo.

Duru ziliarifu kwamba watu wawili wa asili ya kizungu na wenzao ambao idadi yao haikubainika walimvizia mfanyibiashara huyo na kumteka nyara. Afisa mkuu wa kitengo maalum cha polisi mjini Dar es Salaam Lazaro Mambosasa alisema maafisa wa usalama katika eneo hilo wamewekwa katika hali ya tahadhari.

Mohammed ameorodheshwa miongoni mwa mabwenyenye watajika barani Afrika huku jarida la Forbes likisema ana mali ya takriban dola bilioni 1.5.