Pembe za thamani dola milioni-3.1 zanaswa Malaysia

Maafisa nchini Malaysia wamenasa pembe za vifaru za thamani ya takriban dola milioni-3.1 zilizokuwa zimesafirishwa kutoka Msumbiji kupitia Qatar. Akiongea na wanahabari, mkurugenzi wa kitengo cha forodha katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuala Lumpur alisema pembe hizo za uzani za zaidi ya kilo-51 zilikuwa zimepakiwa kwenye kreti na kufichwa katika bohari moja la mizigo katika uwanja huo wa ndege. Pembe hizo zilikuwa zimeingizwa nchini humo kutoka Doha nchini Qatar,kwenye ndege ya shirika la Qatar kwa kutumia stakabadhi bandia. Malaysia ni lango kuu la kupitishia bidhaa za wanyama pori ambazo huuzwa katika mataifa mengine ya bara Asia, ingawa afisa mmoja wa forodha aliwaambia wanahabari kuwa bidhaa nyingi za wanyama pori huuzwa humo. Hata hivyo hakuna mshukiwa yeyote aliyetiwa nguvuni kuhusiana na kisa hicho huku uchunguzi ukiendelea.