Patrick Ole Ntutu akiri kushindwa na Tunai, Narok

Mbunge wa Narok Magharibi anayeondoka Patrick Ole Ntutu ambaye alishindwa kwenye uchaguzi wa ugavana uliokamilika hivi majuzi na Samuel Ole Tunai amekiri kushindwa na kuwahimiza wafuasi wake kukubali matokeo ya uchaguzi akisema tume huru ya uchaguzi na mipaka-IEBC iliandaa uchaguzi huru na wa haki huko Narok na katika taifa lote kwa jumla. Akikiri kushindwa Ole Ntutu alisema yuko tayari kufanya kazi na gavana Samuel Ole Tunai ili kuwaletea maendeleo wakazi wa Narok. Aliwashukuru wafuasi wake na kuwahimiza kudumisha amani na akawashauri dhidi ya kuitikia miito ya kufanya maandamano kutoka kwa viongozi wasioridhishwa na matokeo ya uchaguzi. Mbunge mteule wa Narok-Magharibi Gabriel Ole Tongoyo ambaye alichaguliwa kwa tiketi ya Chama Cha Mashinani alisema yuko tayari kushirikiana na gavana mteule Samuel Ole Tunai ili kuhakikisha wakazi wa kaunti ya Narok wanafurahia matunda ya ugatuzi. Lydia Ntimama ambaye alikuwa akiwania wadhifa wa mbunge wa kaunti kwa tiketi ya chama cha CCM pia alikiri kushindwa akisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki. Ntimama alishindwa na Soipan Kudate.