Papa Francis ataka amani kudumishwa katika mji wa Jerusalem

Papa mtakatifu Francis ametumia ujumbe wake wa kila mara wa krismasi kuitisha amani kudumishwa katika mji wa Jerusalem huku akitoa wito kwa Israel na Palestina kufanya mazungumzo. Alitoa wito wa kutafutwa kwa suluhisho mwafaka ambalo litawezesha mataifa hayo mawili kuishi kwa amani. Rais wa Marekani Donald Trump maajuzi alitangaza kuwa Marekani inautambua mji wa Jerusalem kuwa mji mkuu wa Israel. Hatua hiyo iliibua shutuma kali kutoka baadhi ya mataifa ulimwenguni. Juma lililopita wanachama wa umoja wa mataifa waliunga mkono azimio lisilofungamana na upande wowote kuwa uamuzi wowote kuhusu hadhi ya mji wa Jerusalem halifai. Palestina inataka kutengewa eneo la mashariki mwa Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa lake la usoni. Mataifa mengi yana afisi za balozi zake katika mji wa Tel Aviv.