Operesheni Kubwa Yafanywa Kuwasaka Wanamgambo Wa Alshabaab Waliowaua Maafisa Wa Polisi Mandera

Operesheni kubwa ya kiusalama inaendelea kuwasaka wanamgambo wa alshabaab waliowaua maafisa watano wa polisi katika kaunti ya Mandera. Maafisa hao waliuawa mwendo wa saa tatu unusu jana asubuhi kufuatia shambulizi walipokuwa wakisindikiza basi lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Mandera. Kwenye taarifa, Inspekta jenerali wa polisi Joseph Boinet alisema kuwa wanamgambo hao walivamia basi hilo la Desert Cruiser huko Dimu, eneo la Elwak baina ya Kotulo na Chuma Mrefu. Makabiliano ya risasi baina ya maafisa wa polisi waliokuwa kwenye gari la polisi na wanamgambo hao yalisababisha vifo vya maafisa watano huku wengine wanne wakijeruhiwa lakini maafisa hao waliweza kulinda basi hilo ambalo liliwasili huko Elwak salama pamoja na abiria waliokuwemo. Gavana wa Mandera, Ali Roba, alishtumu kisa hicho akitoa wito kwa maafisa wa usalama kutumia taarifa za kijasusi kutoka kwa jamii ya eneo hilo huku kukiwa na madai kwamba washambulizi hao walionekana kufahamu mienendo ya mabasi na maafisa wa usalama. Roba alidai kwamba wakazi wa eneo hilo walikuwa wameibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa wageni miongoni mwao kabla ya shambulizi hilo kutokea. Shambulizi hilo la jana ni la hivi punde zaidi kwenye eneo hilo linalopakana na Somalia nchi ambayo imeshuhudia mashambulizi mengi ya kigaidi yanayotekelezwa na kundi la alshabaab.