Ongoro akihama ODM

Siku moja baada ya chama cha ODM kuwapatia zaidi ya wawaniaji 800, uteuzi wa moja kwa moja ili kushiriki katika uchaguzi mkuu wa tarehe 8 Augosti, Seneta maalum Elizabeth Ongoro amekihama chama cha ODM, akisema uamuzi wake ni kutokana na hali ya kuhangaishwa. Lakini Ongoro bado hajakitaja chama ambacho amehamia. Hata hivyo, duru zimearifu kwamba anatarajiwa kukitaja chama kipya siku ya Jumatano ambapo atahutubia wanahabari kabla ya chaguzi za mchujo za chama cha ODM zilizopangiwa kuanza Ijumaa wiki hii. Mbunge wa Nyali Hezron Awiti ambaye maajuzi alikihama chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, amejiunga na chama cha a�?Vibrant Democratic Partya�?. Awiti alipokewa na chama kipya, akitaraji kwamba kitampa tiketi ya kuwania kiti cha Ugavana cha Kaunti ya Mombasa. Alikihama chama cha Wiper na kusema alikuwa akihangaishwa na watu ambao hakuwataja na ambao lengo lao ni kumnyima tiketi ya chama cha Wiper. Alighadhabishwa haswa na uamuzi wa katibu mkuu wa Wiper Seneta Omar Hassan, kutangaza pia azma ya kuwania kiti hicho cha Ugavana. Wawili hao watamenyana na gavana wa sasa Ali Hassan Joho, na pia Suleiman Shabhal wa chama cha Jubilee.