Omtatah afika mahakamani kupinga mpango mpya wa ushuru

Mwanaharakati Okiya Omtatah amewasilisha kesi mahakamani akitaka kuahirishwa hatua mpya za utozaji ushuru ilivyopendekezwa kwenye mswada wa fedha wa mwaka huu. Omtatah anasema walipa ushuru nchini sharti walindwe dhidi ya kutozwa ushuru mkubwa ambao haujaidhinishwa na bunge. Anasema utaratibu ufaao haukufuatwa kuafikia mapendekezo kwenye mswada huo kwani ulichapishwa baada ya waziri wa fedha Henry Rotich kusoma bajeti ya kipindi cha mwaka 2018/2019 mwezi uliopita.

Omtatah anasema kumpa Rotich mamlaka ya muda wa kurekebisha sheria za kitaifa kuhusu ushuru kupitia mswada wa fedha bila kupitia utaratibu wa bunge inavyohitajika ni ukiukaji katiba na ni hatua isiyo na uhalali wa kisheria. Kadhalika anasema ingawa mswada wa fedha ulisomwa mara ya kwanza kupitia mapendekezo ya bajeti, mabadiliko mengi ya ushuru yalikuwa ni mapendekezo tu ambayo yalihitaji idhini ya bunge lakini yalianza kutekelezwa baada ya bajeti kusomwa. Kwenye kesi hiyo Omtatah amemshtaki waziri Rotich, kamishna mkuu wa halmashauri ya ukusanyaji ushuru nchini John Njiraini, bunge na mwanasheria mkuu.