Ombi la kuwaondoa majaji wawili wa mahakama ya juu lawasilishwa

Ombi limewasilishwa kwa tume ya kuajiri maafisa wa idara ya mahakama la kuwachunguzwa na kuwaondoa afisini majaji wawili wa mahakama ya juu ambao ni naibu jaji mkuu Philomena Mwilu na jaji Isaac Lenaola kuhusiana na mienendo yao. Kwenye ombi hilo lililowasilishwa na Derrick Ngumu, ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika la Angaza Empowerment Network lililoko Mombasa, inadaiwa kwamba majaji hao walikiuka kanuni za maadili za tume ya JSC wakati wa kesi iliyowasilishwa mahakamani na muungano wa NASA kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa tarehe 8 mwezi uliopita. Amedai kwamba naibu jaji mkuu alikuwa akiwasiliana na seneta wa Busia, Amos WakoA� ambaye ni wakili wa Raila Odinga na James Orengo, ambaye alikuwa wakili mkuu wa upinzani kwenye kesi hiyo. Ngumu anadai kuwa naibu jaji mkuu Mwilu alishauriana kwaA� kina na seneta Wako mnamo tarehe 17 mwezi Agosti mwaka huu, siku moja kabla ya muungano wa NASA kuwasilisha kesi yake katika mahakama ya juu. Alidai kuwa mazungumzo hayo yaliangazia kesi hiyo ya NASA ya kupinga uchaguzi wa urais. Ngumu pia amedai kwamba Lenaola alikuwa akiwasiliana mara kwa mara na mkuu wa sekretariati ya kampeni za mgombeaji urais wa mrengo wa NASA huku kesi hiyo ikiendelea, miongoni mwa madai mengine.