Nzamba Kitonga Afika Mbele Ya Kamati Ya Kuajiri Wahudumu Wa Mahakama

nzamba

Aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya wataalamu kuhusu marekebisho ya katiba hapa nchini Nzamba Kitonga ameahidi kurahisisha utekelezaji haki hapa nchini kwa kuzindua mahakama katika kila eneo bunge endapo atateuliwa kuwa jaji mkuu mpya. Kitonga ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya marekebisho ya katiba Sudan Kusini amesema endapo atateuliwa atashirikiana na tume ya kuajiri wahudumu wa mahakama, majaji na mahakimu ili kubainisha changamoto zinazokumba idara ya mahakama na kuweka mikakati ya kutoa mwongozo wa marekebisho ya idara hiyo katika siku 100 za kwanza kama jaji mkuu.

Akiongea alipofika mbele ya kamati ya tume ya kuajiri wahudumu wa mahakama leo, Kitonga alitaja weledi wake wa kimataifa akisema anastahili kuchukua wadhifa huo. Kitonga ambaye ni wa nne kufika mbele ya kamati hiyo alieleza lengo lake la kubuni mikakati ya teknolojia ya mawasiliano ili kurahisisha utaratibu wa kesi hapa nchini.

Aidha Kitonga alisema iwapo atateuliwa, atahakikisha kuwa katika muda wa miaka mitano taifa hili litakuwa na utaratibu mwafaka wa utekelezaji haki na uteuzi wa majaji na mahakimu ili kuondoa mrundiko wa kesi mahakamani. Kitonga ambaye ana weledi wa kisheria wa miaka 36 amewahi kuhudumu katika shirika la umoja wa mataifa la kuchunguza mauaji ya halaiki nchini Rwanda, mwenyekiti wa chama cha wanasheria Afrika Mashariki na mwenyekiti wa chama cha wanasheria hapa nchini.