Nyumba ya Rais Joseph Kabila yavamiwa ,afisa mmoja kuuliwa

Nyumba ya rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila imevamiwa na afisa mmoja wa polisi kuawa katika kisa hicho. Haya ni kwa mujibu wa baadhi ya wajumbe wa eneo hilo na radio moja inayodhaminiwa na umoja wa mataifa. Picha zilizochapishwa katika mtandao zilionyesha nyumba kuu katika shamba hilo lililoko katika kijiji cha Musienene kaskazini mwa Kivu mashariki mwa taifa hilo iliteketezwa na moto. Kabila hakuwa katika nyumba hiyo wakati wa shambulizi hilo ambalo lilitekelezwa usiku wa siku ya jumapili hadi jumatatu. Haikubainika ni nani aliyehusika na shambulizi hilo. Maiti ya polisi aliyeuawa ilikuwa imeteketezwa. Taifa hilo linakabiliwa na mzozo wa kisiasa unaohusishwa na hatua ya rais Joseph Kabila ya kukataa kuondoka mamlakani baada ya kipindi chake cha kuhudumu kukamilika mwaka uliopita.