NTSA yataka serikali ya Embu kukoma kuwapa wenye Probox nafasi ya kuegesha

Halmashauri ya Uchukuzi na Usalama Barabarani (NTSA) imetoa wito kwa serikali ya Kaunti ya Embu kukoma kuwapa wenye magari aina ya Probox nafasi ya kuegesha magari hayo katika vituo vya mabasi kama njia ya kukomesha matumizi ya magari hayo kwa uchukuzi wa umma. Mkuu wa kitengo cha oparesheni wa halmashauri hiyo Hared Adan amesikitishwa na na ongezeko la matumizi mabaya ya magari kwenye kaunti hiyo ambayo anakariri yanachangia ongezeko la ajali za barabarani katika eneo hilo. Alisema idadi kubwa ya magari ya Probox huhudumu kama magari ya uchukuzi wa umma, huku yakibeba abiria 11 badala ya watano.

Aliongeza kuwa idadi kubwa ya wenye magari hayo wanayatumia kwa uchukuzi wa umma kwa njia haramu. Alisema kwamba watashirikiana na kampuni za bima ili kupiga marufuku utoaji huduma za bima za uchukuzi wa umma kwa wenye magari aina ya Probox. Akiongea wakati wa oparesheni kwenye barabara kuu ya the Embu a�� Kiritiri, Adan alitoa wito kwa abiria kuwa waangalifu kuhusu magari wanayoabiri na kutii sheria za barabarani. Maafisa wa NTSA walikuwa awali mnamo jumatano wamezuru kituo kikuu cha mabas kuwahamasisha madereva na makondakta kuhusu usalama barabarani.