NTSA kuwa na hatua mpya za kupunguza ajali za barabara nchini

Halmashauri ya kitaifa ya uchukuzi na usalama barabarani (NTSA), imetangaza hatua mpya za kupunguza ajali za barabarani kote nchini. Hatua hizo za halmashauri hiyo ikishirikiana na polisi wa trafiki ni pamoja na kuongeza misako dhidi ya watu wanaovunja sheria za trafiki. Hatua hizo zimewekwa huku sheria za sasa za trafiki zikitiliwa shaka katika kukabiliana na ajali za barabarani ambapo zaidi ya watu 170 wameuawa kwenye ajali za barabarani katika muda wa wiki tatu zilizopita. Hayo yanajiri huku halmashauri hiyo ikiimarisha misako yake dhidi ya wavunjaji wa sheria za Traffiki. Katika eneo la Maanzoni kwenye barabara kuu ya Nairobi kuelekea Mombasa, magari yapatayo 30 yalinaswa baada ya kupatikana yakiwa na vidhibiti mwendo vilivyochokorwa. Naibu afisa mkuu mtendaji wa halmashauri ya (NTSA), Hared Adan, amehimiza wale wanaotumia barabara kuwa wangalifu zaidi msimu huu wa sherehe za Krismasi na mwaka mpya.