Nkaissery Ashutumu Vyombo Vya Habari

Wizara ya usalama wa ndani imetahadharisha vyombo vya habari hapa nchini kwa kuchapisha ripoti inayodhalalisha maafisa wa polisi na mashirika ya usalama yanayohusika na juhudi za kukomesha uhalifu hapa nchini. Waziri jenerali mstaafu Joseph Nkaissery alishutumu vyombo hivyo kwa kudai kuwa maafisa wa polisi wamehusika na mauaji kiholela ya wananchi akisema ripoti hiyo haina usawa na kwamba inaonekana kutukuza vitendo vya wahalifu sugu hapa nchini. Akihutubia wanahabari katika jumba la Harambee jijini Nairobi, Nkaissery alieleza kufadhaishwa na juhudi za vyombo vya habari za kubeza huduma ya polisi kwa taifa licha ya mwandishi wa ripoti hiyo kukiri kuwa watu wanaodaiwa kuuawa na maafisa wa polisi walijulikana kuwa wahalifu.

Hata hivyo waziri alisema wizara hiyo imewachukulia hatua za kinidhamu maafisa watoro lakini hiyo haiwezi kutumiwa kama sababu ya kulaani idara nzima ya polisi. Alisema asilimia 90 ya malalamishi dhidi ya matumizi mabaya ya silaha na maafisa wa polisi hayajabainishwa. Haya yamejiri siku moja baada ya gazeti moja la hapa nchini kudai kuwa maafisa wa polisi waliwaua kiholela watu 121 kati ya mwezi Januari na Agosti mwaka huu ikilinganishwa na watu 114 waliouawa mwaka uliopita na kwamba watu 262 wameuawa na maafisa wa polisi tangu mwaka 2015.