Ngilu akatalia mbali shilingi milioni 6 za kuapishwa

Gavana mteule wa kaunti ya Kitui, Charity Ngilu amekatalia mbali shilingi milioni sita zilizotengewa sherehe ya kuapishwa kwake akisema anachohitaji ni Biblia pekee wakati wa shughuli hiyo. Ngilu aliambia kamati andalizi ya sherehe hizo kuwa hakuna haja ya kutumia kiasi kikubwa cha pesa kugharamia sherehe ya siku moja ilhali mamilioni ya wakazi hawana maji safi ya kutumia. Ngilu alisema sherehe ya kuapishwa haitahitaji kiasi kikubwa cha pesa na akaagiza pesa hizo zitumiwe kuboresha huduma za maji kwa wakazi. Ngilu alisema haya alipomtembelea kamishna wa kaunti ya Kitui, Boaz Cherutich afisini mwake kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa. Hapo jana, gavana mteule wa kaunti ya Nairobi, Mike Mbuvi Sonko alikatalia mbali shilingi milioni 25 zilizotengewa kuapishwa kwake. Sonko alisema badala yake, pesa hizo zinafaa kutumiwa kulipa malimbikizi ya mishahara ya wafanyikazi wa kaunti ya Nairobi.