Ngilu akataa kuondoa marufuku ya uchomaji makaa

Gavana wa Kitui Charity Ngilu hataondoa marufuku ya uchomaji makaa katika kaunti ya kitui. Gavana huyo amesema marufuku hiyo itadumishwa ili kukabiliana na athari za ukataji miti, ambao umekithiri katika kaunti hiyo. Ngilu ambaye alifika mbele ya tume ya uwiano na utangamanoA�wa taifa alikanusha madai kwamba alizua uhasama miongoni mwa jamii zinaoishi huko Kitui na pia kuchochea uchomaji mali.

Alisema wachomaji makaa hasa wanaoishi katika sehemu za misitu hawana nafasi katika kaunti ya Kitui na hivi karibuni watafurushwa. Aliandamana na kinara mwenza wa muungano wa NASA ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka aliyesema wanaomshtaki Ngilu wana njama fulani.

Mnamo mwezi Januari, gavana Ngilu kwa mashauriano na kamishna wa kaunti ya Kitui anayeondoka Boaz Cherutich walipiga marufuku uchomaji makaa na uzoaji mchanga katika kaunti ya Kitui kwa masoko ya nje ya kaunti hiyo.