NASA yasema haitashiriki kwenye uchaguzi utakaoandaliwa na maafisa wa sasa wa IEBC

Muungano wa NASA umesema kwamba hautashiriki kwenye uchaguzi utakaoandaliwa na maafisa wa sasa wa tume ya uchaguzi na mipaka IEBC. Muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga umetoa wito wa kujiuzulu mara moja kwa afisa mkuu wa tume hiyo Ezra Chiloba pamoja na maafisa wengine wowote watakaobainika kutosimamia ipasavyo uchaguzi wa urais uliobatilishwa. Muungano huo wa upinzani uliongeza kwamba hautaruhusu karatasi za uchaguzi mpya wa urais kuchapishwa na kampuni ya Al Ghurair yenye makao yake huko Dubai. Upinzani pia ulikosoa chama cha Jubilee kwa kile ulichotaja vitisho kwa idara ya mahakama, ukiongeza kuwa asasi zote za umma ziko huru kuambatana na katiba. Wakati wa ziara yao hapa Nairobi, viongozi wa NASA walishtumu Jubilee kwa kukashifu majaji ya mahakama ya juu, wakisema uamuzi wa mahakama hiyo ulizingatia katiba. Nasa imetoa wito kwa wafuasi wake kujitokeza kwa wingi wakati wa marudio ya uchaguzi huo wa urais.