NASA yapendekeza kuletwa kwa mtaalam wa kimataifa wa teknolojia ya habari

Muungano wa NASA umependekeza kuletwa kwa mtaalam wa kimataifa wa teknolojia ya habari na mawasiliano kuhusu maswala ya uchaguzi ili kusimamia utumizi mwafaka wa mfumo wa usimamizi wa pamoja wa uchaguzi hapa nchini KIEMS  kwa siku zilizosalia kabla ya uchaguzi mkuu.  Kulingana na kigogo mwenza wa muungano wa  NASA Musalia Mudavadi  ambaye aliwahutubia wanahabari leo asubuhi, mtaalam huyo atawawezesha wakenya kuwa na imani na vifaa vya kielektroniki vitakavyotumika wakati wa uchaguzi mkuu ujao.  Muungano huo pia umepongeza tangazo la serikali za Marekani na Uingereza kuhusu hiari yao kusaidia katika uchunguzi ili kubainisha waliohusika katika mauaji ya msimamizi wa maswala ya teknolojia ya  habari na mawasiliano  katika tume ya IEBC Chris Msando. Taarifa hiyo ya NASA imejiri huku tume ya IEBC ikiwahakikishia wakenya kuwa kifo cha  Msando hakitaathiri maandalizi ya uchaguzi mkuu wa wiki ijayo. Kwenye taarifa mwenyekiti wa tume hiyo  Wafula Chebukati amesema shughuli za tume hiyo zitaendelea jinsi ilivyopangwa . Chebukati amesema majaribio ya mfumo wa uchaguzi yaliyopangiwa kufanywa jana yatafanywa kesho saa tisa alasiri.