NASA yaionya Jubilee dhidi ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi

Muungano wa upinzani wa NASA umekionya chama cha Jubilee dhidi ya kufanyia marekebisho sheria za uchaguzi, ukisema hatua hiyo itahujumu ufanisi ambao umeafikiwa katika taratibu za uchaguzi hapa nchini. Kinara waA� NASA, Raila Odinga amesema marekebisho hayo yaliyowasilishwa bungeni na wabunge wa mrengo wa Jubilee kuhusu kuondolewa kwa teknolojia wakati wa uchaguzi, hayanuiwi tu kutimiza maslahi yao ya kibinafsi bali pia ni njama ya kuiba kura kwenye uchaguzi mkuu wa tareheA� 26 mwezi Oktoba. Akiongea na wanahabari katika makao makuu ya Wiper huko Lavington, Odinga alisema upinzani hautanyamaza huku taifa hili likirejeshwa nyuma, ambapo alitoa wito kwa wakenya wajitolee kulinda katiba. Alitangaza kwamba wafuasi wa NASA wataandaa maandamano kote nchini siku za jumatatu na ijumaa kuanzia wiki ijayo kuhakikisha hatua zinachukuliwa ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki. Odinga pia alitofautiana na utawala wa Jubilee kuhusiana na kile alichokitaja kuwa kukamatwa bila sababu kamili kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa wa upinzani, pamoja na kuzuiwa kwa mgombea mwenzake Kalonzo Musyoka kuzuru Uganda katika uwanja wa kimataifa wa ndege wa JKIA jana asubuhi. Odinga alisema upinzani hautakubali vitisho vya aina hiyo dhidi ya viongozi wa NASA.