NASA yafanya kampeni Machakos

Muungano wa  (NASA) ulipeleka kampeini yake katika kaunti ya Machakos ambapo uliwahimiza wakazi wa eneo hilo kuunga mkono upinzani na kuahidi kupunguza gharama ya maisha . Akihutubia mkutano wa hadhara mjini Machakos, vinara wa  NASA walitetea manifesto yao na kupuuzilia mbali madai ya Jubilee kwamba wanawaigiza . Mgombea urais wa muungano huo wa NASA Raila Odinga, alisisitiza kuwa muungano wake umejitolea kutekeleza elimu ya upili bila malipo mnamo mwezi Septemba na kubuni mpango makhsusi wa utekelezaji.  Kiongozi wa chama cha Amani  Musalia Mudavadi alimhusisha meneja wa masuala ya kisheria wa kampuni ya sukari ya Mumias  Leonard Joseph Lubya na makundi ya ulaghai katika kampuni hiyo ya sukari . Mudavadi alidai kuwa Lubya aliuawa kwa kukataa kupakia  sukari iliyoagizwa kutoka nje katika mifuko ya kampuni ya sukari ya Mumias . Aliongeza kuwa makundi hayo yako macho kuona kwamba yanajipatia faida kubwa bila kujali kampuni za sukari za humu nchini . kiongozi wa chama cha Wiper ambaye pia ni mgombea mwenza wa  Odinga, Kalonzo Musyoka alitangaza kuwa seneta Johnstone Muthama ataongoza kampeini za urais za muungano wa NASA katika eneo hilo . Muthama alikuwa ametofautiana na Musyoka kuhusu uwaniaji wa Wavinya Ndeti badala ya  Bernard Kiala ambaye sasa ni mgombeaji huru.