NASA yafanya kampeini zake maeneo ya Rift Valley kusini

Viongozi wa muungano wa -NASA walipeleka kampeini zao katika eneo la Rift valley kusini wakianzia na eneo la Sigor katika kaunti ya Bomet. Wakiongozwa na mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga, kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi na kiongozi wa chama cha CCM Isaac Rutto, viongozi hao walisema kwamba asilimia 45 ya fedha za kitaifa zinapaswa kugatuliwa. Viongozi hao waliozungumza baada ya kufungua mradi wa maji wa Sigor walisisitiza kwamba Jubilee imeshindwa katika ugatuzi lakini watahakikisha kwamba mara tu watakapochukua uongozi watahakikisha ugawaji sawa wa rasilmali. Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi aliikosoa serikali ya Jubilee kwa kufanya kampeini kila mara dhidi ya magavana wa muungano wa NASA badala ya kushirikiana nao kuhakikisha kufaulu kwa ugatuzi. Kiongozi wa chama cha CCM Isaac Ruto alisema ni Raila Odinga pekee atakayehakikisha kuwa ugatuzi unafanikiwa. Kiongozi wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka alimpongeza gavana wa Bomet kwa juhudi zake za kuimarisha huduma za ugatuzi na akaishutumu serikali ya jubilee kwa kukwamisha ugatuzi.A�Viongozi hao aidha walipeleka kampeini zao huko Kapkatet na Suswa huko Narok.