NASA yadai mtandao wa uchaguzi wa IEBC ulidukuliwa, waomba utulivu

Mgombeaji wa muungano wa NASA Raila Odinga amedai kuwa mfumo wa kuwasilisha matokeo wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC uliingiliwa kwa kutumia kitambulisho cha marehemu meneja wa teknologia ya habari na mawasiliano Chris Msando. Akihutubia wanahabari leo asubuhi katika kituo cha habari cha NASA kilichoko katika jumba la ABC mtaani westlands, Odinga alidai kuwa mfumo huo uliingiliwa kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa jana . Alisema kuwa wametoa ushahidi kwa tume ya IEBC kuonyesha jinsi wadukuzi walivyobadilisha matokeo ya mfumo huo kutoka mwendo wa saa 12.37 adhuhuri hapo jana hadi saa nane alfajiri ya leo na wamealikwa kwa mkutano na mwenyekiti wa tume ya IEBC Wafula Chebukati kutoa habari zaidi ili hatua ziweze kuchukuliwa . Pia aliitaka tume ya IEBC kutoa kwa haraka fomu nambari 34A zinazotoa matokeo kutoka mashinani kama inavyohitajika kisheria . Alisema kuwa tume ya IEBC imetoa tu fomu moja ya 34A kinyume cha sheria .
Raila alisema kuwa hawatakubali matokeo yanayotolewa katika mtandao wa tume ya IEBC kwa kuwa matokeo hayo yamefanyiwa marekebisho. Raila alisema kuwa huenda wakaazimia kutoa matokeo yao wenyewe kama walivyoyapokea kutoka kwa mawakala wao iwapo itahitajika na kuwataka wakenya wote kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao za kawaida huku swala hilo likishughulikiwa.